Blog

Maendeleo ya sayansi na teknolojia yamechangia mabadiliko katika utendaji wa kazi mbalimbali ulimwenguni, hali iliyosababisha kuwepo kwa mahitaji ya mafunzo maeneo ya kazi ili kuendana na kasi ya mabadiliko hayo.

Baadhi ya mafunzo yakiwemo yanayohusu tasnia ya habari wakati mwingine huwa ni ghali kwa mwanahabari wa kawaida au chombo cha habari kuyamudu. 

Hata hivyo, wapo wadau wa habari ambao wamekua wakijitolea rasilimali zao kuhakikisha wanahabari wanapata maarifa yatakayowasaidia kuongeza ufanisi kazini na kuhabarisha umma kwa taarifa za kweli na sahihi. 

Miongoni mwa wadau ambao hutoa rasilimali zao kugharamia mafunzo hayo ni pamoja na mashirika ya ndani na nje ya nchini kama Internews Tanzania, Baraza la Habari Tanzania (MCT), Tanzania Media Foundation (TMF), Hivos East Africa, Code for Africa sambamba na kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Africa.

Tofauti na miaka ya nyuma, kwa sasa ili upate fursa ya mafunzo, sehemu kubwa ya wadau huihitaji wanahabari kujaza fomu maalum iliyopo mtandaoni ili kuhakikisha kila mtu anapata fursa hiyo na taarifa zote zinapatikana sehemu moja. 

Matumizi ya teknolojia yanahimizwa katika fursa hizo ili kupunguza gharama kwa muombaji, kuchelewesha maombi, kuongeza ufanisi wakati wa uchakataji, na kupunguza mazingira ya rushwa kwa majaji. 

Licha ya fursa lukuki za mafunzo hayo  kuwepo  kama ya uthibitishaji habari (Fact Checking) na Uandishi wa habari za takwimu (Data journalism) bado kuna makosa ambayo waombaji huyafanya, jambo linalowafanya wakose fursa hizo. 

Miongoni mwa mapungufu au makosa hayo ni pamoja na waombaji kutokuwa makini, kutoambatanisha barua ya utambulisho kutoka kwa mwajiri, uwezo mdogo wa kujibu maswali na kushindwa kufuata maelekezo yanayotolewa na waandaji wa mafunzo.

Kwa kipindi cha miaka sita ambacho Nukta Africa imekuwa ikishirikiana na wadau kutoa  mafunzo, imebainika kwa wachache ambao huzingatia maelekezo wamejikuta wakipata fursa mara kwa mara kutoka kwa mashirika mbalimbali ambayo sehemu kubwa hayahusiani wala kufanya kazi pamoja.

Kama wewe ni miongoni mwa watu ambao wamekuwa wanaomba fursa za mafunzo mtandaoni lakini hawapati, pitia dondoo hizi na uangalie wapi unakosea ili ujirekebishe na wakati mwingine ukipata fursa uipate:

 

Ukosefu wa umakini

Waombaji wengi wakati wa kujaza maombi wamekuwa wanakosa umakini ama kwa kubanwa na muda au kwa kufanya mambo kwa mazoea. Jambo hili limekuwa likiwakosesha nafasi waombaji na hata kuwakatisha tamaa kwa kuwa mara nyingi wamekuwa wakikosa fursa zinazotolewa.

Umakini wako ndiyo unaohitajika hasa unapotaka kuomba na hili siyo tu kwenye maombi yanayotelewa na kampuni ya Nukta Afrika bali ulimwenguni kote. Ni kawaida kukuta muombaji akiandika jina lake ama la taasisi yake kwa herufi ndogo kama juma rajabu badala ya Juma Rajabu.

Wakati mwingine sentensi nzima haina mkato na haijulikani imeanzia wapi na kuishia wapi huku ikiwa na makosa mengi ya kisarufi na kiuandishi kiasi cha kumfanya jaji asielewe kitu. Makosa kama hayo yanasababisha majaji kushindwa kuwachagua waombaji kutokana na ushindani unaokuwepo licha ya ukweli kuwa watu wa namna hiyo  wanahitaji mafunzo.

 

Barua za utambulisho

Sababu kubwa ya watoaji mafunzo kuomba barua kutoka katika chombo chako cha habari ni  kutaka kupata uthibitisho au utambulisho kutoka kwa kiongozi wako wa kazi ili kujua kama unatoka katika taasisi husika na wapo tayari kukuruhusu kuhudhuria mafunzo. 

Kuna wakati mwingine barua hii huwa ni dhamana iwapo kuna mahitaji ya uwajibikaji kama changamoto yoyote ikitokea wakati na baada ya kukamilisha mafunzo. 

Waombaji wasiokuwa na barua mara nyingi hawapewi nafasi hizo. Mbali na barua ya halali uambatanishaji wa barua zilizopitwa muda wake kwa maana zilizotumika katika kuombea mafunzo mengine yasiyohusiana na yanayoombewa pia husababisha mwombaji kukosa fursa. Hii inajumuisha wale wote ambao hughushi barua ilimradi tu wapate nafasi. 

 

Jifunze kujaza fomu mtandaoni

Ili kuongeza ufanisi, waandaji wa mafunzo hata vyuo vikuu kwa sasa wanatumia mifumo wa kiektronikiwa maombi mtandaoni. Matumizi hayo ya mtandao katika uombaji wa fursa za mafunzo ni sehemu ya kuendana na kasi ya mabadiliko ya Tehama ulimwenguni na ndiyo maana Nukta Africa tunasisitiza kila mwanahabari ajue masuala hayo na kutumia mifumo rahisi kama ya fomu zinazotolewa na kampuni ya Google (Google Forms). 

Mwanahabari yeyote anayetaka kupata fursa nyingi zaidi za mafunzo anatakiwa kujifunza namna ya kujaza fomu hizo. 

Kwa kuwa mawasiliano ya waandaji huwa katika tangazo la maombi, omba msaada uelekezwe ili ujaze vema. 

 

Kuzingatia maelekezo

Uzoefu unaonyesha kuwa waombaji wengi hawazingatii maelekezo wanapojaza fomu za maombi. Mathalan, inaweza kuwa ni swali linalomtaka mwombaji kujibu bila kuzidisha maneno 50 lakini mwingine anazidisha.

Wakati mwingine linaweza kuwa ni swali la lazima lenye alama muhimu ambayo lina mtaka mwombaji alijibu bila kuliacha lakini waombaji anashindwa kufuata maelekezo hayo na kufanya tofauti.

Kitendo hicho cha kutozingatia masharti kinamfanya mwombaji akose nafasi ya kuchaguliwa kujiunga na mafunzo husika. Unaweza ukaomba hata mara 1,000 na ukakosa iwapo utakosa umakini na kutoambatanisha viambatanisho muhimu. 

Hivyo, waombaji wakiwemo wanahabari wanashauriwa kusoma fomu ya maombi angalau mara mbili au tatu kabla ya kuanza kujaza maombi yoyote ya mafunzo ili kuweza kuwashawishi majaji na waandaji wa mafunzo hayo kuwachagua.

Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza katika tovuti ya Nukta Habari, unaweza kuisoma pia hapa